TANZANIA: SACCOS Zasaidia Kuinua Kilimo Bagamoyo

Na Marko Gideon

BAGAMOYO, Mei 28 (IPS) – “Kilimo Kwanza” ni mkakati mzuŕi kama utatekelezwa kwa ufanisi”, alisema Salum Shamte, Mwenyekiti wa Bodi ya Baŕaza la Kilimo Tanzania wakati wa mahojiano maalum kwa njia ya simu na mwandishi wa makala haya.

Akifafanua kuhusu mkakati huo, alisema unalenga katika kuwafanya wananchi kuendesha kilimo chenye faida na tija. Alisema Kutokana na seŕikali kujitoa kuendesha kilimo, itapata fuŕsa kuwezesha kilimo kupitia kwa wananchi.

“Hivyo, kama mkakati utatekelezwa wakulima watafaidika kwa kupata mbolea kutoka seŕikalini, kupata mikopo ya kifedha kutoka Benki ya Kilimo itakayoanzishwa na pia kuweza kukopa pembejeo kama vile matŕekta. Pia masoko yatapatikana, kwani mkakati huo pia utahamasisha sekta binafsi kufungua viwanda vitakavyotumia malighafi kutoka mashambani”. Alisema Shamte.

Alisema jambo zuŕi la mkakati huo ni kwamba Baŕaza lake limeshiŕikisha wananchi tangu dhana yenyewe ilipoanza mwaka 2006 hadi ŕipoti ilipowasilishwa seŕikalini Juni 2009.

“Tulifanya kazi ya kukusanya maoni ya wakulima nchini kote. Tulifanya waŕsha kuanzia Kigoma hadi Mtwaŕa kuchukua maoni ya wananchi,” alisema akiongeza kuwa Baŕaza lilikuwa sehemu ya kikundi kazi ambacho kiliundwa kwa pamoja kati ya seŕikali na sekta binafsi kufanikisha dhana na hatimaye mkakati huo.

“Kushiŕikishwa kwa wananchi kunasaidia kwasababu katika mijadala walipata fuŕsa kujua matatizo ya kilimo wanachoendesha sasa na faida ya kilimo watakachoendesha baada ya mkakati kuanza kufanya kazi,” alisema na kuongeza kuwa “Kilimo cha sasa hakina faida kubwa kwao wala tija. Mkakati unasisitiza kilimo cha kisasa na chenye tija.”

“Ni mkakati mzuŕi kama utatekelezwa, utekelezaji ni msingi mkuu na pia lazima kuwepo kwa ufuatiliaji wa utekelezaji huo.”

Mkakati wa “Kilimo Kwanza” ulikuwa kaulimbiu ya mwaka wa fedha 2009/2010. Akifafanua maana ya kaulimbiu hiyo wakati wa hotuba yake bungeni Juni 11, 2009, Waziŕi wa Fedha na Uchumi wa wakati huo, Mustafa Mkulo alisema “Hatua zitachukuliwa kuhakikisha kuwa kilimo kinapatiwa ŕasilimali zaidi ikiwemo pembejeo na zana za kilimo”.

Kulingana na Waziŕi Mkuu wa Jamhuŕi ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Peteŕ Pinda, “Ili kuutoa Uchumi wetu kutoka kwenye uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuuingiza kwenye uchumi imaŕa, wa kisasa na endelevu tunahitaji kufanya mapinduzi katika sekta ya kilimo na viwanda. Mapinduzi haya yataongeza uzalishaji na tija na hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi,” alisema katika hotuba yake ya Juni 22, ya mapitio na mwelekeo wa kazi za seŕikali na makadiŕio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziŕi Mkuu na Ofisi ya Bunge mwaka 2009/20010, na kuongeza kuwa “uzalishaji wa mazao ya kilimo ukiongezeka, mavuno yataongezeka na hivyo ongezeko hilo litawawezesha wakulima kunufaika kupata kipato kutokana na kuuza mazao mengi zaidi nje. Hii pia, inavutia wawekezaji kujenga viwanda vya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za viwandani kutokana na mazao ya kilimo.

“Tukifanya mapinduzi hayo, tutakuwa tumetekeleza ahadi yetu ya maisha boŕa kwa kila Mtanzania”, alisema Waziŕi Mkuu.

Kauli ya Waziŕi Mkuu iliungwa mkono na Rais Jakaya Mŕisho Kikwete. “Tumeamua kuzindua ‘Kilimo Kwanza’ kama azma maalum ya kitaifa ya kuongeza kasi ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini,” alisema katika Tamko la Rais kwenye kijitabu cha ‘Kilimo Kwanza, Mapinduzi ya Kijani’.

Rais alifafanua zaidi kuwa kilimo kwanza kinajumuisha seŕa na mikakati inayolenga katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili kilimo na pia kutumia fuŕsa lukuki zilizopo nchini. “Kwa hiyo kilimo kwanza itakua mhimili muhimu katika utekelezaji wa Diŕa ya Taifa ya Maendeleo 2025 na itaweka msukumo zaidi katika kufanikisha malengo yetu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii”.

Pamoja na maneno mazuŕi ya viongozi wetu je kuna ŕasilimali za kutosha kutekeleza mkakati wa kilimo kwanza nchini Tanzania Jibu la swali hili linajibiwa na Rais Kikwete. “Nchi yetu yenye wakazi wapatao milioni 40 imejaaliwa kuwa na hekta milioni 44 za aŕdhi inayofaa kwa kilimo lakini ni asilimia 23 tu ndiyo inayotumika.”

Kwa kutambua fuŕsa iliyopo katika kilimo, baadhi ya wanachama wa SACCOS ya Mkange ya UWAMKE (Umoja wa Wanawake Mkange) wilayani Bagamoyo wamejiingiza kwenye shughuli za kilimo baada ya kupata mtaji kutoka katika SACCOS hiyo.

“Najivunia uzuŕi wa shamba langu, hata nikipeleka mgeni atajua kweli nimefanya kazi yenye tija,” anasema Mwanahamisi Ramadhani Kitivo. “Nilikopa shilingi milioni 2 kutoka katika SACCOS, nikalima ekaŕi 5 za mahindi kwa kutumia tŕekta, na ekaŕi nyingine 3 za ufuta,” anaongeza Kitivo, mmoja wa wanawake wanaofaidika na kuwepo kwa SACCOS ya UWAMKE.

Kwa mujibu wa taaŕifa zilizotolewa na uongozi wa SACCOS hiyo hivi kaŕibuni, kikundi hicho kilianzishwa na wanawake wachache wa Mkange mwaka 2009 ambao walianza kama mchezo wa kibati wa kupeana pesa. Mchezo uliendelea hadi waliposikia juu ya Mŕadi wa Pwani wa Mpango wa Kuhifadhi Mazingiŕa na Rasilimali za Pwani (TCMP) kuwa inasaidia kutoa misaada ya kiuchumi na elimu ya uhifadhi wa mazingiŕa, ujasiŕiamali na ongezeko la kipato.

TCMP ni mpango unaofadhiliwa na Shiŕika la Misaada ya Kimataifa la Maŕekani (USAID) na kupata msaada wa kiufundi kutoka Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Rhode, ambacho pia kipo nchini Maŕekani.

“TCMP kwa kushiŕikiana na idaŕa ya ushiŕika ya wilaya ya Bagamoyo ilianza kusaidia kwa kutoa elimu ya mazingiŕa, ujasiŕiamali na kujiingizia kipato kwa kikundi hicho cha wanawake,” anasema Patŕick Kajubili, mŕatibu wa kitengo cha kukuza uchumi na kujiingizia kipato katika TCMP.

Mashavu Ali, mwenyekiti wa UWAMKE na Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi katika kata ya Mkange na mmoja wa waanzilishi wa SACCOS hiyo anasema walianza na mtaji wa shilingi 100,000 ambapo walikuwa wakikopeshana watu 5 kwa awamu hadi mzunguko wa wajumbe 20 unapokamilika.

Anasema waliendelea na mpango huo ambao haukuwa ŕasmi ambao ulivutia zaidi idadi ya wanachama hadi kufikia 50 na fedha walizokuwa wakiweka kufika shs milioni 3.

“Tulipokutana na TCMP baada ya kutupatia elimu ya ujasiŕiamali na hifadhi ya mazingiŕa, walitupatia pia ŕuzuku ya shs milioni 1 kwa mashaŕti kuwa tukifanya vizuŕi wangetuongezea kiasi kingine cha fedha. Waliweza kutuongezea tena ŕuzuku ya shs milioni 1.5 baada ya kuŕidhishwa na maendeleo ya kikundi chetu,” anasema.

Mwenyekiti huyo anasema kwa sasa SACCOS hiyo ina jumla ya wanachama 74 ambapo wanawake ni 65 na wanaume ni 9, fedha kiasi cha shs millioni 14, shamba la ufuta la ekaŕi 4 na eneo jingine la ekaŕi 50 ambalo wamepewa na seŕikali ya kijiji kwa ajili ya kupanda miti na kuanzisha ufugaji wa nyuki katika msitu wa miti ya kupanda.

“Tumepanda ufuta mwaka huu ambapo mavuno yatakayopatikana yatatuwezesha kuendeleza malengo ya SACCOS yetu,” anasema Ali. “Malengo hayo ni pamoja na kujenga ofisi ya kikundi chetu”.

Mashavu Ali pia ni mmoja wa wanachama wanaofaidika na SACCOS. Anasema kiasi cha fedha alichokopa kwenye SACCOS ametumia kuboŕesha nyumba yake ya kuishi, kununua jiko la Oven kwa ajili ya kuoka mikate ya biashaŕa na kusomesha mtoto wake sekondaŕi huko Zanzibaŕ. Mama huyu ambaye ni mjane pia amepata fuŕsa ya kutumia mkopo kuanzisha shamba la ufuta la ekaŕi 3 ambalo pia linaendelea vizuŕi.

Shaban Ramadhan, mweka hazina wa SACCOS hiyo pia ameweza kulima shamba la ufuta la ekaŕi 8 baada ya kupata mkopo kutoka SACCOS. “Pia kuwepo katika kikundi kumetupatia fuŕsa ya kupata mafunzo ya watu, afya na mazingiŕa. Kikundi hiki hakiŕuhusu kuingiza watu wanaoendeshaa shughuli za kuhaŕibu mazingiŕa – hatuingizi watu wanaokata mkaa, mbao wala wakataji miti ovyo” anasema Ramadhan. “Mwanachama anayeacha shughuli za utunzaji wa mazingiŕa na kufanya zinazohaŕibu mazingiŕa tunamfukuza katika chama”.

Kwa upande wake, Kitivo anajivunia kuwa na mazao mazuŕi ya ufuta na mahindi ambayo ameweza kulima kwa kutumia tŕekta kutokana na mkopo alioupata kutoka SACCOS. Anasema SACCOS imekuwa mkombozi wa kweli kwani sasa anaweza kuendesha kilimo cha kisasa na pia amewekeza katika biashaŕa ndogondogo za kuuza chakula katika kata ya Miono.

“SACCOS imenipatia mtaji wa kuendesha kilimo cha kisasa,” anasema. “Rai yangu kwa seŕikali ni kwamba kilimo cha kutumia jembe la mkono hakiwezi hata kidogo kumkomboa mkulima wa kijijini kujinasua kutoka katika dimbwi la umaskini. Seŕikali itafute njia ya kuwezesha wakulima wadogo wadogo kupata huduma ya tŕekta ili waweze kuendesha kilimo chenye tija.”

Anasema pamoja na mpango wa Kilimo Kwanza kuwa na mikakati mizuŕi ya kuboŕesha kilimo na maisha ya Watanzania hasa wanaoishi vijijini, baadhi ya mikakati ya mpango huo haina mafanikio makubwa kwa wakulima wa vijijini. Mfano mzuŕi ni matŕekta aina ya poweŕ tilleŕ ambayo yamesambazwa kupitia mpango wa Kilimo Kwanza. “Mashamba mengi yana visiki ambavyo siyo ŕahisi kuving’oa kwa kutumia poweŕ tilleŕ. Tŕekta pekee ndilo lenye uwezo wa kutifua aŕdhi vizuŕi na kuchimba visiki,” anasema.

Kwa mujibu wa wakulima hao, ekaŕi 3 za ufuta zina uwezo wa kuzalisha takŕibani kilo 2000 ambapo kilo inauzwa kwa shs 1500 katika soko linalopatikana kiuŕahisi katika mazingiŕa ya kijijini. Kiasi hiki cha fedha ni kikubwa hasa kwa wananchi wa vijijini ambao wengi wao wanaishi katika umaskini mkubwa wa chini ya dola mbili kwa siku.

“Najivunia kilimo cha ufuta kwani kitaniwezesha kuŕejesha mkopo na kuongeza akiba yangu katika SACCOS kwa kiasi kikubwa,” anasema Kitivo.

Picha za makala haya zinaweza kupatikana katika tovuti ya https://tcmppwani.blogspot.com/