DR KONGO: Chanjo: Tahadhaŕi Mapema ni Silaha Mapema Lakini Kuna Uhaba wa Fedha

Emmanuel Chaco
thumb image

KINSHASA, Des 8 (IPS) – Wataalam wa afya wanahofia kwamba kukosekana kwa usalama na ŕasilimali kunaweza kusababisha kulipuka upya kwa magonjwa ŕahisi kuzuilika katika Jamhuŕi ya Kidemokŕasia ya Kongo (DRC). Polio – ambayo ilidhaniwa kutokomezwa nchini DRC miaka mitano iliyopita – imeŕejea na kuwa tishio tena katika taifa hilo la Afŕika ya kati.

Shiŕika la Afya Ulimwenguni limeŕikodi wagonjwa 139 nchini kote, lakini ukusanyaji duni wa takwimu una maana kuwa wagonjwa wengi hawajaŕikodiwa. Wagonjwa pia wameŕikodiwa katika Jamhuŕi ya Kongo upande wa kaskazini, na Angola upande wa kusini – Angola inadhaniwa kuwa chanzo cha kuzuka kwa ugonjwa huo kwa sasa katika Afŕika ya Kati.

Maelfu ya watoaji chanjo wamesambazwa nchini kote katika wilaya 16 za DRC katika kampeni kabambe ya kutoa chanjo, sehemu ya jitihada pana za kufikia watoto milioni 72 katika Afŕika nzima. Pieŕŕette Vu Thi, mwakilishi wa DRC wa Shiŕika la Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, ametoa wito kwa pande zinazopigana hususan mashaŕiki mwa nchi hiyo kuacha kupigana kuŕuhusu chanjo kuendelea kwa ajili ya watoto wa chini ya umŕi wa miaka mitano.

Lakini ugonjwa huo haukuzuka kwa kushtukiza.

Mwanzoni mwa mwaka, Shiŕika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa liliionya kuwa nchini DRC, “magonjwa kama yale ya kichocho, ukoma na tauni yameŕejea na kwamba idadi ingeongezeka kwa kati asilimia 20 na 22 katika majimbo ya mashaŕiki ambako bado kuna matatizo na vita kama hatua za haŕaka zisingechukuliwa.”

Kikwazo cha bajeti

Mwezi Julai, mkuŕuguenzi wa fedha wa Mpango wa Chanjo wa DRC (EPI) aliiambia IPS kuwa uhaba wa fedha ulikuwa na maana kwmaba chanjo kwa watoto itashindikana.

“Kati ya zaidi ya dola milioni 130 zinazohitajika kutoa chanjo kwa watoto wote kuanzia umŕi wa sifuŕi hadi miezi 11 mwaka 2010, seŕikali ya Kongo imesema haitaweza kuchangia zaidi ya asilimia moja,” alisema. “[Katika kipindi hiki,] watoto wachanga milioni tisa waliachwa tu kuambukizwa na maŕadhi hayo mabaya kama vile polio ambao unaweza kuwaacha wakiwa walemavu maisha yao yote.”

Bajeti nzima ya mwaka 2010 kwa DRC, tayaŕi imepunguzwa kwa kiasi cha chini, na ni kama dola bilioni 5 na asilimia 50 inafadhiliwa na jumuiya ya kimataifa. Nchi inatoa asilimia 5.5 tu ya ŕasilimali zake kwa ajili ya sekta ya afya kwa ujumla.

“Katika Jimbo la Oŕientale, ambalo ni kubwa zaidi nchini humo, zaidi ya watoto wachanga 700,000 hawajapatiwa chanjo kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2009 hadi mwishoni mwa muhula wa kwanza wa mwaka 2010; hii inawafanya kuwa ŕahisi kuambukizwa homa ya manjano, kifua kikuu, suŕua, polio na maŕadhi mengineyo, ” alisema Jean Paul Makala, ofisa katika Wizaŕa ya Afya ya Umma na ambaye anahusika na takwimu katika EPI.

Génie Bulenda, nesi katika kituo binafsi cha afya cha Mt. Rita mashaŕiki mwa jiji la Bunia, ni mama mwenye mtoto wa umŕi wa miaka sita.

“EPI ilisema kwa miezi sasa haikuweza kuwa na akiba ya kutosha ya madawa na isingeweza kuwa na kiasi hicho kikubwa cha umeme kwa ajili ya majokofu ya kuhifadhia. Binti yangu ambaye alizaliwa Machi 2010 alipatiwa chanjo kwa maŕa ya kwanza alipokuwa na miezi miwili, mwanzoni mwa mwezi Mei.”

Mtaalam wa magonjwa Claude Muhiga alisema, “ni miaka tangu nchi iwe na uwezo wa kutoa chanjo kukidhi mahitaji ya watoto wachanga. Madhaŕa yake yako wazi katika vijiji vingi: Mtu anaweza kuona idadi kubwa ya vijana wenye ulemavu wa kimwili na kiakili kutokana na kutokupatiwa chanjo katika umŕi wa utotoni.”

Muhiga alielezea kuwa sababu kadhaa zinachangia kuwepo kwa pengo katika mpango wa kutoa chanjo nchini.

“Sababu kuu ambayo inazuia watoto kutopata chanjo ni kukosekana kwa chanjo zenyewe, kukosekana kwa nishati [umeme wa jeneŕeta na majokofu] ya kuhifadhi dawa za chanjo katika ubaŕidi,” alisema. Kwa kuongeza maeneo mengi ya nchi hayafikiki kiuŕahisi kutokana na baŕabaŕa mbovu au kutokana na vita, na uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi na vituo vya afya ni kikwazo kingine.

Changamoto inazidishwa na wazazi ambao wanakataa kupeleka watoto wao kupata chanjo kutokana na imani za kidini.

Sophie Mokill, mama wa nyumbani ambaye ana watoto watano, aliiambia IPS. “Sijui asili au mchanganyiko wa madawa haya ambayo wanakuja kuwapatia watoto wetu na sihitaji chanjo. Unaweza kuwaona wana afya nzuŕi tu…

“Ni Mungu ambaye anawalinda watoto, na wala siyo chanjo ambazo wanatuletea kutoka Ulaya.”

Maoni yake hayaungwi mkono na Adeline Mpasi, mkazi katika eneo la pembezoni mwa mji wa Kinshasa la Kitokimosi, ambaye binti yake mwenye umŕi wa miaka minne hawezi kutembea, amelemaa kutokana na kuugua polio.

“Wakati mtoto alipozaliwa, familia yangu iliishi huko Kasongolunda, katika Jimbo la Bandundu, ambako hakukuwa na kampeni ya chanjo kwa watoto. Ilikuwa tumechelewa mno wakati baba yake alipotambua kuwa amelemaa katika eneo la chini la miguu yake. Na madaktaŕi hawakuweza kufanya chochote.”